Tatizo
linalojitokeza Mtwara isichanganywe na laana za rasilimali zinazoikumba
bara la Afrika. Huu ni mwamko mpya ambapo wananchi wanatambua haki zao
za msingi na kuamua kuyapigania, hasa rasilimali zao kwa lengo la
kujikwamua kutoka kwenye umasikini unaowakabili. Serikali iliyo
madarakani isiingize pamba masikioni na kuligeuza swala la kupingwa na
wananchi kuwa la kisiasa. Ni vyema serikali ikajitathmini kwa umakini
mkubwa na pia ikaheshimu maoni ya wananchi ili ijiokoe
Desturi ya
kutengeneza mikataba mikubwa kwa usiri na viongozi wa umma wasio na
maadili, imewaletea wananchi wa Tanzania matatizo makubwa ya kiuchumi.
Tatizo la Mtwara ni zao la udanganyifu kwenye mikataba yetu. Ni tatizo
linalotoa nafasi ya kipekee kwa serikali yetu kujitathmini na kupitia
upya sera zake za kiuchumu na uwekezaji, ambazo zimekuwa kandamizi,
danganyifu na isiyo na tija kwa raia wa Tanzania.
Kuna baadhi
yetu ambao wanaweza kuyafananisha migogoro nchini Kongo na Nigeria na
maandamano ya Mtwara. Kwa hakika Migogoro ya Kongo na Nigeria ni
tofauti na huu wa Mtwara. Wa-kongo na Wanaigeria ni makundi ya
kipiganaji ambayo yapo kwenye mapambano na serikali zao. Wanapigania
uongozi na utawala wa nchi. Ni watu wenye silaha nzito zinazolenga
kuzing’oa serikali zao, tofauti na wana mtwara wanaopigania haki na
maendeleo ya kiuchumi. Wana Mtwara wanapinga ufisadi na dhuluma
inayoendelezwa na serikali kupitia maandamano ya amani
Wana
Mtwara ni raia wa kawaida wasiokuwa na silaha yoyote isipokuwa nafsi
zao. Wakufunzi wa historia watakubaliana nami kwamba, katika historia ya
dunia, hakuna jeshi ambayo imeweza kuishinda nguvu ya umma, hasa pale
wananchi wanapoamua kupigania haki zao kutumia njia ya amani. Mfano wa
ufisadi unaopingwa na watu wa kusini mwa Tanzania ni ule wa gharama ya
ujenzi wa bomba la gesi. Kwani vyombo vya habari vimenukuliwa vikisema
kwamba, tathmini ya
ujenzi
kutoka mtwara hadi Dar-es-salaam, ilikuwa ni dola za kimarekani
600millioni, lakini cha ajabu, mwisho wa siku gharama hiyo imeongezeka
na kufikia dola za kimarekani 1.2billioni.
Wananchi hawawezi
kunyamazia ufisadi kama huu. Na kwa mwenendo huu, nguvu yao inazidi
kuongezeka na hakuna chochote ambacho serikali inaweza kukifanya
kujinasua. Ni bora serikali ikakiri makosa na kuwashugulikia mafisadi
waliojiusisha na huu hujuma dhidi ya watanzania. Kwani mwisho wa siku,
hiyo hasara atakayebebeshwa ni mtanzania ambaye amechoswha na dhuluma
pamoja na umasikini. Siyo fisadi aliyeficha fedha Uswisi
Ugunduzi
wa mafuta nchini Kanada umewaletea neema ya kiuchumi wananchi wa jimbo
la Alberta, na uchumi wa Kanada kwa ujumla. Malipo ya dola 120 za
kimarekani kwa lisaa limoja kwa wahitimu wa sekondari, ni ya kawaida.
Wakazi wa Alberta wanafurahia rasilimali zao. Makampuni ya mafuta
yanashiriki kikamilifu kusaidia miradi ya kijamii. Lakini katika hali ya
kusikitisha kule Tarime (Nyamongo) wakazi wa maeneo yale wamekuwa
masikini zaidi ya walivyokuwa kabla ya wawekezaji kuchukua ardhi yao.
Vyanzo vyao vya maji vimechafuliwa na havifai tena, mifugo na hata
baadhi ya wakazi wanakufa na mangonjwa yasiyojulikana
Umasikini,
ukiwa, na ukosefu wa ajira unatawala Tarime, kwani hata wachimbaji
wadogo wadogo hawana ardhi tena ya kuchimba, huku wageni wakipewa ajira
ndogo ndogo kama za kuendesha malori ya mchanga ambazo zingefanywa na
wazawa wa Tarime. Inasikitisha kuwaona Wakenya, Wa Afrika Kusini, Wa
Kanada na Wa Australia wakiendesha hayo malori huku wakazi wa Nyamongo
wakionekana kama adui kwenye ardhi yao. Na hayo ndio baadhi ya matatizo
ambayo serikali yetu imeyafumbia macho, hasa serikali inapoamua
kuwatumia polisi kuwaua raia wanaodai haki yao ya kupata riziki.
Wana
Mtwara wanaandamana kudai maendeleo ya kiuchumi. Watu wa kusini
wameiona gesi asilia kuwa ndio njia pekee ya kujikwamua kutoka kwenye
umasikini. Wameshuhudia ndugu zao kule Tarime wanavyonyanyaswa na
serikali na hata kuuwawa na polisi. Hawataki tena ahadi. Wanachokita ni
utekelezaji utakao boresha maisha yao. Serikali isifanye kosa ya
kupuuzia haya madia . Wasithubutu kuyaletea siasa au kajaribu kutumia
nguvu ili kuwaziba midomo wanaharakati wanapinga gesi kupelekwa
Dar-es-salaam, badala yake, serikali iwe makini katika kutafuta chanzo
cha matatizo na suluhisho la kudumu
Serikali makini itajiuliza
maswali ya msingi kama vile ni kwa nini wananchi hawataki gesi
isafirishwe kwenda Dar-es-salaam. Katika kujitathmini, bila shaka
itapata majibu mbalimbali . Itagundua kwamba tupo katika nyakati
tofauti. Wakati wa kizazi cha Intaneti, hasa vijana wenye muamko na
hamasa wasiotaka kuwatwika wengine lawama ya matatizo yanayowakabili.
Serikali itagundua kizazi cha kipekee kisicholaumu wengine kwa ufukara
wao. Kizazi kisichoogopa mabomu ya machozi, maji ya kuwasha au risasi za
moto. Kizazi kisichoshabikia uomba-omba. Serikali itagundua kizazi
kinachotaka kujikwamua kutoka kwenye umasikini kutumia rasilimali na
vipaji vyao.
Ni kizazi kipya kinachotaka ajira, elimu bora,
huduma bora za afya na miundombinu inayoridhisha. Ninamaanisha kizazi
kinachoelewa wazi kwamba, WACHINA hawana upendo nao, ila WACHINA
wanapenda rasilimali zao. Watu wa kusini wamegundua kwamba hadithi za
Abunuwasi haziishi, na uhakika wa kuishi maisha ya neema ni lazima
yaanzie kwao wenyewe kwa kuamka kutka usingizini. Na kwa hakika,
wanakusini wameamka. Na kama serikali haitashugulikia madai yao, basi
mwisho wa hiyo serikali siyo swala la mjadala. Wanakusini wamegundua
kwamba, ni lazima “waamke” na kujitegemea badala ya kusikiliza ahadi
ambazo wamekuwa wakiyasikia kwa miaka 50 iliyopita.
Waheshimiwa
Mwakyembe, Kagasheki, Magufuli na Muhongo wanajulikna kuwa wachapakazi
wasiowaonea aibu majambazi ya kiuchumi -Mafisadi-. Lakini hawa viongozi
wakiendelea kufanya kazi katika mazingira ya kuzungukwa na majambazi
ndani ya serikali, na wanasiasa wasiokuwa na nidhamu katika kusimamia
rasilimali za umma. Basi watabaki kuwa mateka wa mafisadi ingawa wengi
wa hao mafisadi, serikali inawahamu.
Kizazi cha simu za mikononi
na ujumbe mfupi, na mitandao ya kijamii wameamka kutoka usingizini, na
kasi yao ni ya kutisha. Hakuna wa kuwazuia. Hawataki propaganda za
kisiasa na misaada ya KICHINA ambayo mara nyingi ndio chimbuko la
ufisadi tunayoiona nchini kwetu, kama hiyo ya Mtwara. Wametambua
wanayoyataka na kwa muda wanaoutaka wao. Maandamano ya Mtwara ni moto
utakaosambaa kwa kasi. Ni moto wa UAMSHO. Unawaamsha wananchi waliolala
kujua haki zao za kimsingi. Serikali ijitathmini na kuyashugulikia kero
za wananchi mapema. Mafisadi wasipewe nafasi kuiyumbisha nchi
Mungu Ibariki Tanzania