Historia ya muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava kama unavyojulikana
miongoni mwa wengi hivi leo una historia ndefu. Ni historia ndefu kiasi
kwamba hivi leo wengi hatukumbuki tena hata muziki huu ambao hivi leo
umetokea kuwa kipenzi cha wengi ulianzaje,ukapitia hatua na harakati
gani mpaka kufikia hapa ulipo hivi leo.
Miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo wa harakati za mwanzo kabisa za muziki
wa bongo flava ni aliyewahi kuwa DJ maarufu nchini Tanzania kwa jina
Mike Pesambili Mhagama(pichani).Mike sio tu miongoni mwa mashuhuda wa
mwanzo bali pia ni miongoni mwa watu wachache walioamini katika muziki
wa kizazi kipya tokea mwanzo.Kumbuka hizo ni zile enzi ambapo muziki huo
ulikuwa ukichukuliwa kama “uhuni” tu na sio aina mpya ya muziki au
burudani.Ni watu wachache sana walioweza kutabiri hatua ambazo muziki
huo ungepiga miaka kumi au kumi na tano baadaye.
Lakini pia Mike amekuwa akikerwa na jinsi ambavyo kumekuwepo na
upotoshwaji au upindishwaji wa vipengele fulani fulani muhimu vya
historia ya muziki huo. Katika kujaribu kuiweka vyema historia hiyo,Mike
Mhagama ameandika kwa mapana na utulivu wa kina kuhusu harakati za
mwanzo za muziki wa kizazi kipya,suluba walizopitia yeye na watangazaji
wenzake katika kuutambulisha muziki huo,wadau mbalimbali anaowakumbuka
katika harakati hizo,wanamuziki wenyewe,promoters wa muziki nk.
Pia Mike Mhagama,anaweka wazi kitu ambacho watu wengi wamekuwa
wakijiuliza;Nini chanzo cha neno Bongo Flava? Nani mwanzilishi wake?Kwa
jibu hilo na historia nzima,kwa jinsi anavyoikumbuka Mhagama, msome
kuanzia hapo chini,kwa maneno yake mwenyewe, kama tulivyoyanakili kutoka
katika blog yake(kwa ruhusa na baraka maalumu).Habari imegawanyika
katika sehemu nne ili iwe rahisi kwako kuzisoma na kuelewa vyema
anachokizungumzia Mike Mhagama. Mwenyewe anasema yawezekana kabisa asiwe
sahihi kwa asilimia zote na ndio maana anapenda kukaribisha hoja,maoni
na masahihisho yoyote kutoka kwako msomaji.Mike Mhagama hivi sasa
anaishi huko Los Angeles,California nchini Marekani.
CHIMBUKO LA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA NA MAANA HALISI YA NENO BONGO FLAVA.
Moja kati ya mambo niyapendayo mno maishani ni muziki.Nimekuwa
mfuatiliaji mzuri sana wa muziki si tu ule wa nje lakini kwa karibu ule
wa nyumbani hasa muziki wa dansi na ule wenye umaarufu sana hivi sasa
ujulikanao kama Bongo Flava (Muziki wa Kizazi Kipya).Katika mapenzi hayo
imekuwa kama bahati kuwa mmoja wa vijana wengi tuliobahatika kuuona
muziki huu wa kizazi kipya ukizaliwa na pengine bahati zaidi bila kusita
kusema;kuwa mmoja kati ya wale tulioanzisha kusukuma gurudumu la
muziki huu kufikia hapa ulipo na nafasi yake kutambulika si tu Afrika
Mashariki bali pia kwa sasa duniani kwa ujumla.
Kama ilivyo kwa aina zingine za muziki Tanzania,mfano muziki wa dansi
basi utakuwa mkosefu wa fadhila bila kujumuisha majina kama Patrick
Balisidya,Mbaraka Mwaruka Mwinshehe,Salum Abdalah na hata Remmy
Ongara.Hawa ni vinara na walifanya kila wawezalo kuja na ubunifu si tu
kuvutia wateja wao bali kuutangaza muziki wao ndani na nje ya nchi na
kuipa Tanzania kitambulisho chake kwenye jukwaa la sanaa ya muziki.Kazi
za wanamuziki hawa zilifana sana kwa ushirikiano mkubwa na chombo
ambacho kwa Tanzania ni muhimu sana katika kueneza au kutambulisha kitu
kipya,RADIO.Watangazaji kama Mzee Ibrahim Chimgege,Enock
Ngombale,Timothy Pata,Abisai Stephen,Seif Salum Nkamba na Julius
Nyaisangah chini ya ma-bwana mitambo mahiri kama akina James Mhilu na
Crispin Lugongo wanastahili pongezi kwa kiasi kikubwa katika kurekodi na
kusimamia mitambo wakati wanamuziki hawa wakitafuta majina na namna ya
kujitambulisha kwa jamii itakayosikiliza muziki wao.Bahati mbaya
huwasikii sana watu hawa katika zinazoitwa historia kwa sababu wengi ni
rahisi kuwasahau lakini mchango wao ni mkubwa sana na unastahili
heshima hasa unapoandika au kuizungumzia historia ya muziki wa dansi
Tanzania.
Nimetoa mfano wa hali halisi kwa ufupi kuhusu muziki wa dansi ili kukupa
nafasi ya kujua kwa undani kile ambacho kinakweza kichwa cha habari
hapo juu.Nia yangu hasa ni kuandika yale niliyoyaona na uzoefu wangu
katika muziki huu wa sasa maarufu kama Bongo Flava.Muziki huu umeshika
kasi na unapendwa sana hivi sasa kila kona.Ni faraja kuona hata wale
walio ughaibuni siku hizi si ajabu kumkuta mtu ana albamu jpya la
mwanamuziki wa Bongo Flava akiicheza ndani ya nyumba yake au garini kwa
fahari.Inafurahisha kuona mapenzi kwa muziki huu yamekuwa makubwa na
hilo ndilo lengo kuu.
Pamoja na yote haya,kama ilivyo kwa kila jambo ni vyema historia yake
ikawa nyoofu na si kama ilivyo sasa ambavyo imekuwa ikipindishwa
pindishwa mno,sijui kama ni kwa makusudi au kwa wengi kutojua harakati
na wanaharakati walioufikisha muziki huu hapa ulipo.Kwa kuandika kwa
usahihi yale yaliojiri juu ya chimbuko la muziki huu tutakuwa
tunawatunzia wanetu na wengineo haki ya kuuelewa na kuutukuza zaidi
muziki huu na msimamo wake katika jamii ya leo na ijayo.Shukrani labda
nizitoe kwa Kaka Bonny Makene na Uncle michuzi kwa kunisukuma kujaribu
kuandika nikijuacho juu ya muziki huu.
Kama nilivyododosa hapo juu kuhusu muziki wa dansi basi sasa niingie
kwenye muziki huu wa kizazi kipya.Muziki huu ni ule ambao unajumuisha
mitindo mbali mbali ambayo zamani tulizoea kuona ikipigwa na watu wa nje
ya Tanzania kuanzia Hip Hop,R&B,Zouk na hata Soul.
Katika Hip Hop ya Tanzania pia utakosa fadhila kama hutotaja vijana wa
mwanzo kabisa ambao kuanzia mivao yao na kufoka foka kwao kulikuwa ni
burudani na ushawishi tosha kwa watu kuanza kudadisi kuhusu maana halisi
ya utamaduni huu hasa Tanzania.Kwa wakati huo ilionekana kama uhuni
tena wa kupita kiasi.Nitawataja wachache ninaowakumbuka ambao kila
kukicha ukigongana nao kwenye Night Clubs,Samora Avenue pale Salamander
basi ulikuwa unachoka mwenyewe.Nakumbuka vijana kama John Simple,Dj
Rusual,The BIG One,Babu Manju,David Nhigula,Abdulhakim
Magomelo,Kessy,Ibony Moalim,Tom London,OPP (now Jay P) na Dj Ngomeley.
Tukiendelea hao niliowataja hapo juu walikuwa chachu katika uvaaji wa
kihip-hop na katika kughani na sijui kama kuna mtu atasahau watu kama
Fresh XE Mtui,BBG (alianza na Mr II),Adili kumbuka,KBC (Mbeya
Tech),Saleh Jabir,Samia X,THE BIG,Rhymson,2Proud.Deplowmatz na wengineo
wengi ambao walikuwepo na wakighani katka school parties au matamasha
ya mtaani kabla hata ya kurekodi nyimbo zao studio.
Kwa mara ya kwanza pia promoters kama Joe Kusaga na Abdul hakim Magomelo
walionekana kutobaki nyuma katika ukuzaji wa sanaa hii ambapo
waliandaa matamasha mbali kama Yo! Rap Bonanza na Coco beach Bottle
Parties kwa ajili ya kuwapa nafasi wale wenye uwezo wa kughani.Matokeo
yake yalikuwa ya kufurahisha kwani kila mmoja alikuwa na shauku ya
kuingia katika gemu.
Kwa vile sio watu wote walikuwa na uwezo wa kughani lakini pia kulikuwa
na wale wenye kuimba kama wanamuziki wengi wa Marekani kwa kupitia
matamasha mbali mbali kwenye Jumba la utamaduni la Urusi,Korea na
mengineyo yalikuwa yakiandaliwa hasa na wanafunzi wa shule mbali mbali
za sekondari jijini kama Forodhani pia matamasha yaliyokuwa yakifanyika
kando kando ya ufukwe ambako wengi wenye kutaka kuimba
walijitokeza.Hapa tunakumbuka kundi kama la Mawingu na mwana dada
Pamela,mwanadada Stara Thomas na Judith Wambura ambao uwezo wake wa
kughani na kuimba kama Mc Lyte ulimpa tafu hasa alipofanya hivyo kwa
mara ya kwanza ndani ya kipindi cha DJ show ya Radio One,shukrani kwa
Ipyana Malecela Mkwavi (RIP) kwa zawadi ya LP yenye instrumental (ala)
tupu aliyonipatia kama zawadi aliporudi toka UK kwani instrumental ya
single “Keep,Keeping on” ndiyo iliyomtambulisha Jay Dee wa leo Radioni
kwa mara ya kwanza japokuwa kabla ya hapo alikuwa mwimbaji wa kwaya
kanisani lakini mweye kusita kuingia kwenye muziki wa kidunia.Pia Kundi
la R&B lililojulikana kama Four Krewz Flava pia Herbert Makange
ambaye pia alikuwa akiimba.
Naweza nikawa nimesahahu majina machache hapo juu lakini kwa ufupi hao
ni baadhi ya watu wa mwanzo kabisa kuuingiza masikioni mwa jamii muziki
wa kizazi kipya pengine hata kabla ya chombo kilichoipaisha juu
zaidi..RADIO.Na ninaposema Radio simaanishi Radio nyingine bali Radio
One Stereo kama Radio pekee yenye kujivunia juu ya ukuaji wa muziki huu
wa kizazi kipya kufikia hapa ulipo.
Lakini uko nako hakukuwa na mteremko,mambo yalikuwa mengi na mazito
mpaka muziki kujipenyeza na kukubalika.Je nini kilichochea mapambano ya
kuuchomeka muziki huu Radioni na kuupa nafasi ya kupigwa sambamba aina
zingine za muziki kama ule wa dansi nk? nani alihusika katika harakati
hizo na nini kilifuata? ugumu huo ulitokana na nini?
Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1994 kituo cha Radio kilikuwa kimoja tu
kinachomilikiwa na serikali na wanamuziki wengi wa awali Tanzania
walitambulika kutokana na nyimbo zao kupigwa katika kituo hicho hasa
kwenye vipindi mbali mbali hasa kipindi maarufu cha kilabu Raha Leo
Show.Japokuwa hakukuwa na mfumo maalumu wa mahojiano na wanamuziki ndani
ya Radio Tanzania lakini kipindi hiki kilionekana kumaliza karibu kila
kitu katika utambulishi wao jkwaani na mpaka jina la mpiga ala au
sauti wanazoimba kutoka safu ya mbele,kati hata nyuma.Mara nyingi
onesho hili lilikuwa likifanyika LIVE.
Wanamuziki ninaowazungumzia ambao walipewa nafasi kwenye kipindi kama
hiki ni wale waliokuwa wakipiga muziki wa dansi na pengine taarabu na
kwaya japo hawa hawakuwa na nafasi sana wakati huo.
Mara baada ya serikali kulegeza masharti kidogo kwenye soko
huria,hatimaye watu binafsi waliruhusiwa kuanzisha Radio binafsi na kwa
kuanzia walipewa masafa mafupi kwanza kwa sababu za kiusalama na kupima
uwezo wa kumiliki na kuendesha chombo hiki muhimu.
Moja kati ya Radio hizo za mwanzo kuanzishwa ni Radio One Stereo
iliyokuwa ikipatikana katika Megahartz 99.6 FM na kuanzishwa kwa kituo
hiki ama kwa hakika ilikuwa ni mwisho wa ukiritimba na ushindani ulianza
rasmi.Baadhi ya watangazaji waanzilishi ambao waliombwa na mmiliki
ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Mzee Reginald Abraham Mengi ni
Mikidadi Mahamoud ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vipindi na
Utangazaji,Charles Hillary aliyekuwa Mtayarishaji Mkuu wa vipindi na
baadaye Mratibu wa kituo na Julius Nyaisangah aliyesimamia vipindi vya
burudani na usomaji habari.Hawa wote walitokea Radio Tanzania Dar Es
salaam.
Mchango wao kwa watangazaji chipukizi ni mkubwa na haupimiki kwa wale
ambao walipitia mikononi mwa hawa wakongwe bila shaka watakubaliana
nami.Walihimiza kufanya kazi kitaaluma ,walitoa mafunzo na nidhamu ya
hali ya juu tuwapo kazini juu ya utangazaji.Hakika walifunguaa ukurasa
mpya kwenye kitabu cha utangazaji Tanzania.
Darasa la kwanza kuajiriwa mwaka 1994 lilikuwa na chipukizi kama Taji
“Master T” Liundi,Deo “Best Friend” Mshigeni,Flora Nducha na Runkim
Ramadhani Nyamka.Kila mtu alipewa angle/nafasi yake ya kujidai na
kipindi anachoweza kumudu.Mfano Taji Liundi alikuwa katika vipindi vya
muziki vyenye kutoa maudhui na elimu juu ya mitindo mbali mbali ya
muziki na fashion,Taji alikuwa ni mchambuzi.Runkim “Zipompapompa” Nyamka
yeye alikuwa mcheza muziki DJ fundi na alikabidhiwa vipindi vile vya
ufundi wa kuchanganya muziki na mara nyingi wakati wa Weekend.
Radio lianza kukua kwa kasi huku Radio zingine zikianzishwa kukuza
ushindani.Hivyo kituo kilihitaji darasa lingine kupambana na ushindani
huo na darasa hilo lilikuja mwaka 1995 likinijumuisha mimi,Sunday
Shomari na Peace Kwiyamba.Binafsi nilipewa jukumu la kusaidiana na Taji
Liundi katika uchambuzi ndani ya vipindi mbali mbali,Sunday Simba
Shomari alishirikiana na karibu kila kipindi kuleta mchangayiko na Peace
alishirikiana kwa karibu na Deo “Best Friend” Mshigeni katika vipindi
vya salamu na muziki wa taratibu.
Lakini mbali ya vipindi vya burudani uongozi wetu hapo baadaye uliona ni
vyema baadhi yetu tukasoma taarifa za habari na kuripoti kupitia
vipindi vya Current Affairs kama Nipashe n.k.Peace Kwiyamba na miye
tulibahatika kuingia katika upande mwingine wa kituo na kuwa wasomaji
kamili wa taarifa ya habari na maripota.Tulipata mafunzo yetu pale Radio
Tanzania Dar Es Salaam chini ya wakufunzi kutoka chuo kikuu cha
Whitwatersand kilichopo Afrika kusini.Mafunzo haya yalidhaminiwa na
serikali kwa pamoja na mfuko wa Ebert Stiftung nchini Tanzania.
Taji “Master T” Liundi alikuwa ni kivutio cha aina yake si tu kwa uwezo
wake wa kuchambua mambo mbali mbali,bali pia kwa mahojiano yenye ukina
na wanamuziki mbali mbali,uwezo wake wa kuongea lugha zaidi ya tatu na
kwa ubunifu.Ikumbukwe yeye ndiye mwanzilishi wa neno “Chombeza”,neno
alilolibuni kumaanisha kubembelezana kiaina kati ya wapendanao hasa
nyakati za usiku alipokuwa akipiga kipindi maalumu cha nyimbo za
taratibu.Neno hili sasa ni maarufu sana huko Tanzania.
Master T pia alikuwa na ushawishi mkubwa sana hasa kwa vijana ambao
wengi walikuwa ni wasikilizaji wa vipindi alivyokuwa akiviendesha Radio
One.Aliwalenga pia vijana waliokuwa na mwelekeo wa kuingia katika
muziki wa kizazi kipya na hakusita kujitolea kuwashauri kwa ukaribu na
hata kujichukulia muda wake wa ziada kushiriki kwenye mazoezi na wakati
mwingine hata kuwalipia sehemu hizo za mazoezi.Kwa vile sasa tulikuwa
timu moja Taji alinishirikisha sana katika mambo mbali mbali yahusuyo
kazi na hata nje ya kazi.Tulikuwa bega kwa bega kwenye matamasha mbali
mbali yaliyokuwa yakiandaliwa na vikundi vya utamaduni vya shule mbali
mbali za sekondari jijini.
Kwa ukaribu huu mkubwa kati yangu na Taji nia hasa ilikuwa ni
kubadilisha mtazamo wa muziki Tanzania kwani mpaka wakati huo ni nyimbo
za Marekani na nchi zingine za Afrika ndizo zilizokuwa zikichukua
nafasi katika Radio One’s Top Ten,Chaguo la msikilizaji na DJ Show
vipindi ambavyo vilikuwa ni jahazi na vilibeba sura ya kituo.Vipindi
hivi tuliviendesha kwa umahiri mkubwa huku tukipokezana na mwenzangu
Master T.
Mabadiliko haya tuliyokuwa tukiyalenga ni yalikuwa hasa ni kujaribu
kuupa nafasi muziki wetu hasa ule wa kizazi kipya katika show kubwa
nilizozitaja hapo juu,lakini piajitihada zetu hazikuwa na mteremko hata
kidogo bali vikwazo pia,vikwazo hivyo vilimweka Taji katika wakati
mgumu zaidi na kufanya ajiulize mara mbili mbili kwamba yuko kwenye
Radio yenye mabadiliko kwa manufaa ya nani zaidi kama si kizazi kipya?
Nitatoa aina mbili ya vikwazo tulivyokumbana navyo kati ya vingi ambavyo
havikutaka kutoa nafasi kwa wanamuziki wetu wa kizazi kipya kuutangaza
muziki wao.Na vikwazo hivi zilifanya yeyote aliyetaka kwenda kinyume
aidha kupoteza kazi,kusimamishwa kazi au kupewa onyo kali kwa maandishi.
Mosi: Kutokana na mpangilio wa vipindi na kwa matakwa ya watayarishaji
wakuu ilikuwa ni marufuku kupiga muziki wa ndani ya Tanzania zaidi ya
ule wa dansi bila muziki huo kusikilizwa na mmoja kati ya watayarishaji
na kuukubali.Zaidi ya hapo ni ruksa kupiga muziki wowote kutoka Afrika
au Marekani mradi tu uwe ni clean version (toleo lisilo na lugha
chafu).
Na Pili: Si ruksa kufanya mahojiano na mwanamuziki wa kizazi kipya au
asiyefahamika bila mwanamuziki huyo kufanyiwa usaili na watayarishaji
(nikiwa na maana wakongwe) niliowataja hapo juu.
Hayo ni machache tu,lakini yalituweka katika wakati mgumu sana.Kitu
kimoja tulikubaliana na watayarishaji ni suala la kutopiga muziki weneye
matusi na sote tulilipinga hilo lakini kwa haya mengineyo hatukuwa
katika level sawa.Wengi tulionelea kuwa pengine tunarudishwa enzi ya
Radio Tanzania bila kujua na tulipanga kupigania hilo kwa nguvu zote.
Mimi na Taji tulipata barua kadhaa za onyo na hata kuhamishwa vipindi
wakati fulani.Lakini hilo halikutuzuia kuongea kwa sauti juu ya kile
tulichoona si haki.Tulitaka uhuru zaidi kwenye vipindi tulivyokuwa
tukiendesha ili kipindi maarufu kama Top Ten yetu ipambwe na muziki wa
kizazi kipya na mchanganyiko wa miziki ya aina zingine.Hiyo ilikuwa ni
ndoto yetu kila kukicha.
Kwa jitihada hizi za kupigania muziki huu wa kizazi kipya uende hewani
sambamba na aina zingine za muziki bila ukiritimba au masharti uituweka
katika nafasi mbaya kiasi sio kazini tu bali hata mitaani ambako baadhi
walituona kama tunaiga sana u-Marekani na kwamba kwa kutaka kupiga
nyimbo kama hizi za kizazi kipya basi sisi ni wahuni tu na labda lengo
letu kuu lilikuwa ni kutaka kuwafurahisha watu wa makundi yetu tu,kwa
mtazamo wao watu wa makazi ya hali ya juu kama Oysterbay,Masaki n.k bila
kujua binafsi nilikuwa nikiishi (Mbagala Kwa Makuka) mbali kabisa na
maeneo wanayoyasema.Lakini lengo letu lilikuwa ni kutenda haki kwa kila
mwanamuziki hata kama wa kizazi kipya bila kujali wasifu wa
wanakotokea.Japokuwa mwanzo wao ulikuwa mgumu kwani mashairi katika
nyimbo zao yalikuwa lege lege na kutokana na ufinyu wa viwango vya
studio wakati huo midundo/mipigo ndani ya miziki yao ilionekana kutokuwa
na mpangilio,lakini tulihoji kwa nini wasipewe nafasi tu kwanza halafu
tuone jamii itawapokea vipi? ilikuwa si sahihi kukataa kuiga nyimbo
zao na kufanaisha viwango vya urekodi na vile vya wanamuziki wengine wa
kimataifa ambao nyimbo zao mpaka zilikuwa zikichosha.
Mambo yalikuwa magumu na yasiyotabirika kutokana na harakati
hizi.Hatimaye Master T aliondoka Radio One na kwenda jijini Mwanza
ambako Radio (Radio Free Africa) nyingine ilikuwa ikianzishwa.
Baada ya Master T kuondoka nilikabidhiwa vipindi vitatu mfululizo (DJ
Show,Chaguo La Msikilizaji,na Top Ten) kuviendesha,kati ya hivyo DJ Show
ilikuwa weekdays na vingine weekly,ilikuwa mshtuko na kwa kweli kazi
ngumu lakini kwa vile nilipenda na bado naipenda sana kazi ya utangazaji
sikusita kuendeleza kasi ile ile aliyoiacha Taji japokuwa siwezi
kusema kuwa pengo lake lilizibika.Lakini tulikuwa bado tukibadilishana
mawazo kila mara tukiongea kwenye simu akiwa Mwanza.Moja kati ya
msisitizo katika kila mazungumzo yetu ilikuwa ni kukaza uzi na kamwe
kutotetereka na yeye akianzisha mzimamo kama aliouacha huko Mwanza.
Mambo yalianza kubadilika na nadhani kwa sababu ya wakati pia.Makundi
tuliyokuwa tukiyapigania ni makundi mawili makubwa na haya ni makundi ya
mwanzo kabisa katika muziki wa kizazi kipya Tanzania ukiachilia mbali
wale waliokuwa wakighani au kuimba bila kurekodi.
Kulikuwa na makundi ya Hip Hop kama Fresh XE Mtui,Kwanza
Unit,Deplowmatz,Hard Blasters,Gangstar With Matatizo,Wagumu Weusi
Asilia,Young Da’ Mob,II Proud,Saleh Jabir,Samia X,Bugz Malone,Sos B,Afro
Reign na flava kama za akina Mohd Momella,4Kruz Flava,Stara Thomas,
Pamela na Mawingu Band,Connie Francis,Jungle Crewz Posse,Kamakazi
Soldiers(6-7 years old kids),Mac Mooger,E-Attack,Afro Reign (chini ya
Seba Maganga),Bantu Pound,Hardcore Unit/immeditation Kingdom nk.
Pia kulikuwa na makundi ya Reagge kama Inno Nganyagwa,Pompidou,Kimbuteh
& Roots Band,Justin Kalikawe,Innocent Galinoma (USA),Jontwa
Jokeri,Makoya Man na wengineo.
Tusahahu kuwa hata muziki wa dansi uliingia katika kizazi kipya kwa kasi
tofauti kabisa na kubadili mtazamo wa bendi kama Msondo na
Sikinde.Nazungumzia band ya Diamond Sound,wana ikibinda Nkoi chini ya
Eliston Angai.
Wakati pengine hawa makazi yao yalikuwa Dar Es salaam ambako pia studio
nyingi zilikuwepo,tukumbuke pia mikoani kulikuwa na ma-rapa waliokuja
juu ile mbaya.Kwa vile nilisoma mkoani mbeya namkumbuka Rapa aliyekuwa
akiitwa BBG ambaye alikuwa kibwagizo tosha kwenye ma-disco mjini Mbeya
kama RTC,Mount Livingstone,AA Cool Para wa Zanzibar,Comtish wa ZNZ,pia
kundi la Bombastic nk.
Naweza kusema hawa ndio waliweza kufungua ukurasa mpya wa muziki wa
kizazi kipya Tanzania na baadhi yao waliwahi kufanya mahojiano na Taji
kabla hajaondoka kuelekea Mwanza na sio siri walikubalika japokuwa
muziki wao ulianza kupigwa lakini sio sana kama ambavyo piganio letu
lilitaka.
Japokuwa jitihada zilianza kuzaa matunda,kazi sasa ilikuwa kwa
wanamuziki wenyewe kuhakikisha wanauweka ulimwengu wa Tanzania sawa na
kwamba jitihada na harakati zetu za kuupigania muziki huu uende hewani
haziangushwi na kushindwa kwao.Tuliwaasa kupiga muziki wa kueleweka
wenye maadhi si ya ki-Marekani zaidi au nje zaidi bali muziki wenye
mtazamo wa kitanzania.
Tulishauri kuwa ili muziki uwe na nafsi basi ni vyema tukaweka vionjo
vya kwetu zaidi kama wenzetu wa Afrika ya Kusini na mtindo wao
Kwaito.Hata huko Marekani kulikuwa na mtindo tofauti kidogo wenye
mahadhi ya hip hop ulioanzishwa na mkongwe Teddy Riley unaoitwa “New
Jack Swing” ambao ulibaki kam Hip Hop ila yenye vionjo tofauti na ladha
ya New York.Nilitoa mifano hii makusudi kwenye kipindi maarufu
nilichokuwa nikiendesha cha DJ Show kwa sababu walengwa na wadau wengi
wa muziki Tanzania walikuwa wasikilizaji wakubwa wa kipindi hiki.DJ show
ndio ilikuwa kilabu Raha Leo Show yao na nilisisitiza sana kwenye
mapinduzi ya kuwa na mtindo wetu mpya wenye ladha yetu wenyewe.
Kwa vile kwa namna moja au nyingine harakati zilionekana kuanza kuzaa
matunda,nami niliona ni vyema nikauchukua mwanya huu kuzaa kile ambacho
mwenzangu Master T alikuwa mstari wa mbele kukingia kifua ili
kufanikisha azma ya kuwaweka vijana wa Tanzania na muziki wao wa kizazi
kipya mbele ya watanzania lakini huku kukiwa na msisitizo wa “cha
kwetu”.
Nilibahatika kufanya mazungumzo na mmoja wa wana Hip Hop mahiri nchini
anayetokea kwenye kundi la Kwanza Unit Kibacha “KBC” Singo ambaye
tulikuwa tukifahamiana kwa muda mrefu toka mkoani Mbeya ambako sote
tulikuwa tukisoma miaka ya mwanzoni ya tisini.KBC alikuwa ni msomaji
mzuri na muelewa wa mambo mengi ya Hip Hop.
Nilimweleza azma yangu ya kujaribu kuuingiza muziki huu hewani lakini
kwa ushauri wa nini kifanyike ili tusichekwe kwa kuonekana tunaiga sana
umarekani.KBC alicheka lakini alikubaliana nami na kusema hatuwezi
kuibadilisha Hip Hop kufuata midundo yetu lakini tunaweza kuibadilisha
kulingana na lugha pia vionjo vya kwetu.Lakini kwanza KBC alisema si
kila mtu anaweza kufanya Hip Hop na lazima anayetaka kuingia katika game
lazima ajue misingi ya muziki wenyewe.Nilikubali maoni ya KBC na
niliuomba uongozi wa Radio one kugawa saa nzima,kuanzia saa 12 mpaka saa
moja jioni katika siku moja ya wiki ili kutimiza haja hiyo,hasa hasa
kuutenga muda huo kwa muziki wa Rap/Hip Hop tu na si kitu kingine ili
kuupa muziki huu nafasi zaidi ya kusikika na kutambulika tofauti kabisa
na ule wa kutoka The Bronx,Dirty Dirty South au South Central L.A.
Niliomba kwa uongozi ili KBC aongoze kipindi hicho lakini uongozi kwa
sababu za kueleweka ulikataa na kunitaka niendeshe kipindi hicho mimi
mwenyewe na KBC awe mgeni maalumu au mtoa mada katika kipindi hicho
wakati wowote akiwa na nafasi.Kipindi kilikwenda hewani kwa mara ya
kwanza na KBC alikuwa regular.
Matokeo yalikuwa mazuri kwani vijana wengi walikipokea kwa mikono miwili na kushukuru mchango wa KBC katika kipindi hiki.
Hip Hop ya Tanzania ilianza kubadilika na kuanza kuwa na sura na
mwelekeo wa Tanzania kama tulivyotarajia kwani kwa mara ya kwanza mkali
mwingine wa Hip Hop Ramadhani “Chief Rhymson” Mponjika alitoa single
yake kwa kumshirikisha mkongwe wa miondoko ya dansi aitwaye Hassan
Seyvunde na kibao ambacho kilitamba sana sio kwenye Radio tu hata kwenye
TV kutokana na maudhui yake.Pia kundi lao la Kwanza Unit walikubali
mwito na kuibuka na kibao kiitwacho Msafiri ambapo rekodi ilikuwa na
kiitikio kilichodurufu rekodi ya mkongwe wa muziki wa dansi Tanzania al
maarufu kama Mzee Mzima King Kikii Mwanza Mpango.King Kikii naye
alijumuika na familia ya Kwanza Unit katika matamasha mbali mbali
kuwapiga tafu na mara wimbo huo ulipopigwa katika matamasha hayo mapokeo
yalikuwa ni ya kuridhisha na huo ndio ukawa mwanzo wa Hip Hop ya
Tanzania kupanda chati na kukubalika zaidi.
Wakati haya yote yanatokea mkongwe mwingine kwa jina la 2Proud (sasa
Sugu) naye hakuwa nyuma alitoa nyimbo ambazo zilikuwa gumzo na zenye
ujumbe wa moja kwa moja kwa viongozi wa siasa Tanzania mpaka aliyekuwa
Mratibu wa vipindi wa Radio One Charles Hillary alianza kukubali kazi za
wasanii wa kizazi kipya na kuamua kuvunja baadhi ya masharti ambayo
hapo mwanzo yalikuwa ni kikwazo.Charles Hillary kwa mara ya kwanza
alikubali kupiga wimbo wa msanii wa huyu IIProud uitwao “Ni Mimi” katika
moja ya vipindi ambavyo alikuwa akiviendesha.
Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri na upanuzi mkubwa kwa muziki wa Hip Hop
Tanzania ambao sasa ulianza kushamiri kila kona na kwa kasi kubwa.
Lakini changamoto haikuwa kwenye Hip Hop ya Tanzania tu bali hata muziki
wa dansi nao ulianza kubadilika kutokana na wakati.Kama ilivyo kwa KBC
na mchanganuo wake wa mawazo kwenye kipindi changu cha Rap time
ambacho sio siri kiliwafungua macho vijana wengi waliotaka kuingia
katika muizki katika miaka ya 90 ukiachilia wale wakongwe,basi katika
dansi nako kulikuwa na mapinduzi yake.
Sote tunakumbuka bendi kama Diamond Sound ambayo ilikuwa ikipiga nyimbo
nyingi za Congo na zikiimbwa kwa lugha ya kilingala.Niliwahi kumwalika
kiongozi wa band hiyo Elliston Angai katika kipindi cha DJ Show na rapa
wake mashuhuri Allan Mulumba Nkashama na kufanya nao mazungumzo ni
namna gani wanaweza kushirikisha vionjo vya Tanzania zaidi katika
nyimbo zao na Rap zao.Bila kusita walikaribisha wazo hilo na kama
ilikuwa ni mgongano wa mawazo kumbe nao walikuwa wanatafakari namna ya
kutawala soko la muziki wao kwa kuuza CD ambazo muziki wake utakuwa na
mtazamo na ladha ya Tanzania.
Allain Mulumba kutokana na ubunifu wake alikuja na rap yake ya kwanza
kabisa baada ya changamoto hiyo kwenye DJ Show ambayo alitumia tangazo
la sabuni kuonesha muonjo huo.Tangazo lile lilikuwa na maneno kama
“Omari mbona unajikuna sana,sio siri mamaa! ninawashwa sana ngwarariii
ngwararaaa”.
Ndipo sote tulipokubali maapokezi ya muziki na kwa kutumia lugha yetu
kumbe unalipa.Ukumbi wa Silent Inn ulilipuka kwa furaha ya Rap hiyo
ambayo kwa mara ya kwanza ilipigwa usiku huo na kutambulishwa
rasmi,mashuhuda wenzangu katika mapinduzi haya usiku huo pale Silent Inn
walikuwa waandishi wenzangu Sebastian Maganga (Radio One),Farouq Karim
(ITV Zanzibar),John Ngahyoma (ITV Dar) na Chacha Maginga (sasa TBC1)
.Baada ya hapo tulishuhudia band nyingi zikiiga sana mtindo huu na
kuibuka na rap za kiswahili kwenye miziki waliyokuwa wakipiga ambayo ina
asili ya Congo.Tunakumbuka bendi kama FM Musica na zingine ambazo
zilifuata nyayo.
Nanyambulisha haya kwa makusudi ili kuweka kumbukumbu sawa na kwa vile
kuna kusahahulika kwa matukio muhimu kama haya hasa inapofika wakati
wa watu aidha wasiojua kumbukumbu hizi au kwa makusudi ya kukidhiana
wanaandika zinazoitwa historia juu ya mabadiliko ya muziki wa kizazi
kipya Tanzania bila ya kutaja mambo muhimu kama haya.
Na nikiri wazi kuwa pamoja na kuwepo kwa kipindi cha DJ Show ambacho ni
cha kwanza kutambulisha muziki huu wa kizazi kipya hewani na kuwa
kipindi pekee chenye heshima hiyo kabla ya kingine chochote,hivi leo
husikii wengi wakikipa heshima yake na pengine kukisahau kabisa katika
kumbukumbu za muziki huu tunaousheherekea hivi leo.Waulize wanamuziki
wakongwe katika anga za muziki huu watakwambia ukweli huu.Pia kumekuwa
na kusahaulika kwa waandishi wa kwanza kabisa kuandika habari za
wanamuziki hawa kwenye makala na hata kuwafanyia mahojiano kwa mara ya
kwanza.Waandishi kama Angetileh Osiah,Tom Kirumbi,Albert Memba ,Ibra
Poza,Issa Michuzi au Juma Pinto.
Tukirudi kwenye Radio lazima nikubali baadaye pia kulikuwa na upinzani
na vituo vingine ambavyo navyo viliendeleza muziki huu wa kizazi kipya
kwa kasi kubwa sana.Pia watayarishaji wa muziki kama Enrique “Rick”
Figueredo wa Sound Crafters pale Temeke,Joakim “Master Jay” Kimario wa
MMJ Production,Boniphas “Bonny Luv” Kilosa wa Mawingu Studios,Paul “P”
Funk wa Bongo Records (alianzisha kundi la vijna wa miaka saba
lililopiga HipHop),Marlon Linje wa Don Bosco studio.Shukurani kwa
kipindi cha Dr Beat chini ya KBC na Dj Bonny “Luv” Kilosa na Othman “OJ”
Njaidi ambao waliendeleza libeneke katika mtindo ule ule wa ushindani
lakini tukiwa marafiki wa karibu na kubadilishana mawazo mara kwa mara
kwani sote lengo letu lilikuwa moja.Dr Beat ilikuwa chini ya Clouds FM.
Pia wadhamini na mapromota ambao walikuwa na moyo wa dhati katika
kuendeleza sana hii ya muziki wa kizazi kipya.Na upozungumzia muziki huu
basi huwezi kumsahahu Joseph ‘Joe” Kussaga na Abdulhakim Magomelo.
Lakini mimi binafsi mbali ya mkongwe Taji Liundi ambaye alifungua njia
ya mapambano na harakati ili kuupa muziki huu nafasi yake kama ilivyo
dansi na aina nyengine ya muziki,kamwe sitomsahahukijana mwenye akili
“Genius” Dj Sebastian Maganga ambaye alipokea kwa dhati mikoba ya DJ
SHOW baada ya miye kuachia ngazi.Sebastian ana nafasi ya pekee sana
katika muziki huu tangu alipojiunga na Radio One toka Radio
Tumaini,ikumbukwe pia Sebastian ni mwana HipHop aliyetoka na kundi la
Afro Reign toka miaka hiyoo.Sebastian ni mbunifu na ndio yeye
aliyenisukuma zaidi katika kuibadili DJ Show moja kwa moja na kuachana
na nyimbo nyingi za Marekani katika kipindi cha DJ SHOW na pole pole
tuliweza kufanikiwa kwa kushirikiana na DJ Jumanne kutoka Holland ambaye
alitutengenezea promo nyingi za kipindi na kubadili usikivu wa kipindi
hiki kutoka muziki wa Snoopy Dogg/Dr Dre mpaka ule wa akina Mr
II/Kwanza Unit.
Na katika kufanikisha hilo kwa vile DJ Show ilikuwa inapiga muziki
mchanganyiko lakini wa kileo.Siku moja tukiwa kwenye kipindi Sebastian
aligusia mfumo wa kutenga muziki katika dakika 30 kila genre,kama
tunapiga Reggae basi alishauri iwe dakika 30,kama R&B ya Tanzania
basi tutenge dakika 30 nk.Nilikubaliana na wazo hilo kwani lingetufanya
tutoe nafasi sawa kwa kila aina ya mtindo na sio upendeleo wa kupiga
Hip Hop au R&B tu masaa yote mawili ya kipindi.
Ilipofika dakika 30 za muziki wa R & B,siku hiyo nilikuwa kwenye
usukani na kwa mbwembwe nilicheza nyimbo ya kundi la R&B lililoitwa
4Krewz Flava na baadaye kuiunganisha na nyimbo nyingine ya Unique
Sistaz.Kwa vile midundo,mpangilio,lugha na utaalamu wa muziki wenyewe
kamwe huwezi kuufananisha na ule wa Soul 4 Real au SWV kutoka
Marekani,tulipenda tutofautishe kidogo kati ya aina hizi mbili na ndipo
session hii niliibatiza jina ambalo lingetofautisha R&B ya Marekani
na ile ya kwetu….niliipa session hii jina la BONGO FLAVA.
Hii ilikuwa mwaka 1996 na ndio ulikuwa mwanzo wa neno BONGO FLAVA likiwa
na maana muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye vionjo na ladha ya
Tanzania na si vinginevyo lengo kuu ni kuitofautisha na muziki ule wa
Marekani.Hip Hop ya Tanzania ilibaki na itabaki vile vile kama
ilivyo,ila muziki wowote ule wa nje,mbali ya Hip Hop na DANSI ya
Tanzania niliuita na kuufahamishakwa umma wa watanzania kama BONGO FLAVA
ndani ya kipindi cha DJ SHOW cha Radio One.
Nikifikia tamati ya mtazamo wangu na jinsi nilivyoshuhudia muziki huu
ukikua pengine kumekuwa na ubishi ambao kwa maana halisi nimeonelea nao
niudodose kidogo hii leo.Nilipokuwa nyumbani Tanzania nilipata bahati
ya kutembelea Clouds FM ambako mwenzangu Sebastian Maganga sasa ni Mkuu
wa Vipindi na aligusia suala hili la chimbuko zima la muziki huu na
neno BONGO FLAVA.Niliweka haya unayoyasoma wewe hapa bloguni kama
yalivyo na niliomba yeyote mwenye kuona tofauti na ninauona ukweli
kujitokeza lakini hakutokea mtu kupinga.
Nasema hivi kwa vile huko nyuma kuna waliodiriki kujitokeza/kujitangaza
hapo mwanzo na kudai kuwa neno hili BONGO FLAVA ni jina lililotokana au
kutungwa na wao,kitu ambacho mimi na mwenzangu Sebastian Maganga
tunakipinga kwa sababu tunajua ukweli uko wapi.Watu hawa (tunafahamiana
fika) waliombwa kuja studio za Clouds FM siku hiyo katika mahojiano
maalum na kuuthibitishia umma juu ya dai lao lakini hakuna aliyetokea.
Ni kweli kila mtu na mtazamo wake katika kila jambo kutokana na
alivyolishuhudia lakini ni vyema tukawa wakweli kidogo bila kupindisha
mambo pale tunapotaka kuuhabarisha umma juu ya yale tunayotaka
wayafahamu.Katika mnyambulisho huu hapa juu sio lengo wala nia yangu
kumsuta mtu na inawezekana kabisa kama binadamu wa kawaida kuna mambo
nimeyasahau,kama ndivyo basi ni vyema tukasahihishana ili kurekebisha
mambo na sio kudanganya kwa kudhani ukweli kamwe hautojulikana na ndio
maana nimeamua kuandika haya ili kuweka yale ninayoyajua wazi kwa faida
ya kizazi kijacho na hata cha sasa ambacho kimekuwa kikipotoshwa na
wachache.
Na kwa kufanya hivi sina nia hata kidogo ya kutaka au kuuukwa
umaarufu,kwani nimekuwa maarufu toka nina miaka 19 na sihitaji wala
silazimishi kuwa maarufu hivi leo.
Ieleweke kuwa haya yote ni katika kutoa elimu kama shuhuda wa mapinduzi
ya muziki huu Tanzania kwani kumekuwa dhahiri na upotoshaji wa makusudi
au wa kutojijua inapokuja katika mambo muhimu yanaohusu muziki wa
kizazi kipya Tanzania.
Kwa mfano neno hili la BONGO FLAVA lilizaliwa na kutokea katika kipindi
cha DJ Show na si vinginevyo kama ambavyo imekuwa ikidaiwa katika
zinazoitwa historia za muziki huu wa kizazi kipya kutoka vianzio mbali
mbali.
Mfano mwingine hai ni ule kuwa kuna kuna wanaosema TANZANIA MUSIC AWARDS
imeanzishwa na mwanamuziki James Dandu (ambaye alikuwa ni rafiki yangu
mkubwa) lakini watu wanasahau kuwa TANZANIA MUSIC AWARDS ilianzishwa
na mwanamuziki wa zamani wa bendi ya Mawenzi/Prodyuza John Kagaruki
chini ya kampuni yake ya Serengeti Production kwa kushirikiana na
BASATA mwaka 1997 na sherehe za kwanza kabisa ambazo zilirushwa live na
kituo cha ITV zilifanyika pale Whitesand Hotel.
Ni kweli mwaka uliofuata sherehe hizi hazikufanyika tena na
zilipwaya.Lakini tusisahau kuwa mwaka 2000 kampuni ya Look Promotion kwa
kushirikiana na Clouds FM walifanya tena onesho hili ikiwa ni mara ya
pili kufanyika Tanzania.Na mwaka uliofuata bia ya Kilimanjaro kwa
kushirikiana na mwanamuziki James “CJ MASSIVE” Dandu na kampuni yake ya
Dandu Planet walizindua upya sherehe hizi ambazo zimekuwa zikifanyika
kila mwaka toka wakati huo.
Mifano kama hii na mingineyo mingi tu inaleta mushkeri hasa
inavyopotoshwa kwa makusudi ilhali mashuhuda wake tupo tena tukiwa hai.
SEHEMU YA MWISHO
Kufikia hatua hii basi labda niseme tu kuwa imefika wakati wanamuziki wa
Hip Hop na Bongo Flava leo hii wana nafasi yao katika jamii ya
Tanzania na wanapaswa kuenziwa,kukumbukwa na kuheshimika bila
kuchanganya aina hizi mbili za muziki kwani ni vitu viwili tofauti
kabisa lakini lengo likiwa moja.Kuna mambo mawili ambayo nadhani
yakifanyika basi angalau kumbukumbu ya wale wakongwe walioanzisha
harakati na mapinduzi katika muziki huu watadumishwa na wale wapya
watajifunza kutokana na kuwaenzi wakongwe hawa.
Hapa tusisahau pia wakongwe waliokuwa wakipiga ianyoitwa Hard Core
HipHop kama Fresh XE ambaye sidhani kama alibahatika kurekodi,Samia
X,GWM,E-Attack,Underground Soul,Hasheem,KU Crew,Nigga One,D-Rob au II
Proud na wengineo ambao walikuwapo hata kabla ya kipindi cha DJ SHOW au
Radio One kuanza lakini hawakuwa na sehemu ya kuutangaza muziki
wao.Hawa kamwe hawatasahaulika na wana heshima kubwa sana kwenye muziki
wa kizazi kipya nchini Tanzania.
Bila kutegemea “Awards” ambazo zinaonekana kuwa na dosari kila
zinapofanyika kila mwaka kwa tuhuma za upendeleo nadhani imefika wakati
mwafaka kwa muziki huu na wanamuziki wake kuwa na tuzo zake maalum
zitakazofanyika kila mwaka na kuzitofautisha kabisa na zile tulizozioea
za muziki mchanganyiko.
Kuwepo na utaratibu wa kujumuisha wiki ya tuzo hizo na usaidiaji wa
jamii kwa wakongwe watakotumikiwa tuzo hizo kutembelea baadhi ya shule
za msingi au sekondari na kutoa changamoto ya maisha na elimu juu ya
muziki huu kwa ujumla kwa kizazi hiki kijacho.Pia hata kushiriki nao
katika shughuli za usafi wa mazingira kwa siku hiyo.Huu ni mchango tosha
na ishara kuwa muziki huu si uhuni ni sehemu ya maisha kwa kizazi
kipya.
Vile vile sehemu ya mapato na udhamini wa onesho hili iende kusaidia
shule masikini au ya watoto wasiobahatika na wenye ulemavu wa namna moja
au nyingine.
Kwa kufanya haya na mengineyo mengi muziki huu sio tu utakuwa ni wenye
kujijengea heshima bali kuweka kumbukumbu kubwa ya mapinduzi kwenye
ulimwengu wa muziki Tanzania na hadhi yake kuwa ni ile isiyofutika kwa
urahisi machoni na akilini mwa kizazi cha sasa na hata kile kijacho kwa
muda mrefu.
No comments:
Post a Comment